Na Victor Abuso,
Vlabu vya Tanzania bara Simba na Azam FC vipo katika harakati za kuwatafuta makocha watakavyonoa vikosi vyao msimu ujao, baada ya makocha wa timu hizo kufutwa kazi.
Kumekuwa na taarifa kuwa huenda kocha wa zamani wa Taifa Stars Kim Poulsen akizunguziwa kuwa huenda akawa kocha wa vijana hao wa mtaa wa Msimbazi.
Uongozi wa Azam FC mabingwa wa msimu uliopita umetangaza kumrejesha kocha wake wa zamani Stewart Hall.
Duru kutoka Mtaa wa Msimbazi zinasema kuwa Poulsen anayefundisha Silkeborg IF ya Ligi Kuu ya Denmark anatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam kutia saini mkataba na klabu hiyo.
Pamoja na hayo, jina la kocha wa zamani wa Harambee Stars ya Kenya Adel Amrouche raia wa Ubelgiji limetajwa na ripoti zinasema kuwa huenda akawa naibu wa Poulsen.
Amrouche, alikuwa jijini Dar es salaam wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba na sasa habari zinaeleza kuwa atafanya kazi na Poulsen, anayetajwa kuchukua mikoba ya Mserbia Goran Kopunovic.
Kuhusu Azam FC, kocha Hall anarejea kuchukua mikoba ya Joseph Omog kutoka Cameroon aliyetupiwa virago katikati ya msimu uliopita kwa madai ya mwenendo mbovu wa timu.
Mwenyekiti wa Azam, Said Muhammad alisema Hall alikuwa miongoni mwa makocha 12 walioomba kibarua cha kuinoa timu yao.