Na Victor Abuso,
Kamati ya utendaji ya Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF, imeamua kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa Mart Nooij apewe changamoto ya kufaulu kucheza fainali za michuano ya CHAN mwakani, akishindwa aondoke.
Nooij raia wa Uholanzi ambaye kikosi chake hakikufanya vizuri katika michuano ya kusaka taji la COSAFA baina ya mataifa ya Kusini mwa Afrika na kuondoka bila ya kupata ushindi wowote.
Michuano ya CHAN huwahusisha wachezaji wanaocheza soka katika vlabu vya nyumbani barani Afrika na michuano ya mwaka 2016 itachezwa nchini Rwanda kuanzia mwezi Januari.
Tanzania kwa mara ya tatu imejumuishwa katika kundi moja na Uganda kufuzu katika michuano hiyo na mchuano wa kwanza utapigwa katikati ya mwezi ujao huku ule wa marudiano ukiwa mwezi Julai.
Mwaka 2009 wakati michuano hii ilipofanyika nchini Sudan, Tanzania ilifuzu katika michuano hiyo baada ya kuifunga Uganda mabao 3 kwa 2 lakini mwaka 2014, Uganda waliibuka washindi baada ya kuwachabanga Tanzania kwa jumla ya mabao 3 kwa 1 na kufuzu katika fainali hizo nchini Afrika Kusini.
Mbali na Tanzania, mataifa mengine ya ukanda yatakayokuwa viwanjani kutafuta kufuzu katika michuano hiyo ni Djibouti itakayocheza na Burundi huku Ethiopia ikimenyana na Kenya.
Rwanda imekwishafuzu kwa sababu wao ni waandaji.
Viongozi wa soka barani CAF, walikuwa jijini Kigali juma lililopita kuthathmini maandalizi ya michuano hiyo na kusema kuwa yanaendelea vizuri.