Na Victor Abuso,
Yanga FC, mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu huu, watakabidhiwa kitita cha Shilingi za Kitanzania Milioni 80 na Laki Nne baada ya kushinda taji hilo.
Wafadhili wakuu wa ligi hiyo kampuni ya simu ya mkononi Vodacom, wamethibtisha hilo na kuongeza kuwa Azam FC waliomaliza katika nafasi ya pili watapata kitita cha Shilingi Milioni 40, huku Simba FC iliyomaliza ya tatu ikikabidhiwa Shilingi Milioni 28.
Mkuu wa kitego cha Uhusiano mwema katika kampuni hiyo Matina Nkurlu amedokeza mwishoni mwa juma kuwa mfungaji bora msimu huu Simon Msuva kutoka Yanga FC naye atapata Shilingi Milioni 5.
Kipa bora naye atapata Milioni 5 sawa na mchezaji bora wa mwaka huku kocha bora na mwamuzi bora pia watatuzwa.
Wafadhili wa ligi Tanzania bara wanasema wanatoa zawadi hizi ili kuinua kiwango cha soka na kuhimiza ushindani na kutafuta vipaji miongoni mwa vijana nchini humo.
Sherehe ya kuwatuza washindi wa ligi msimu huu zitafanyika katikati ya mwezi wa Juni jijini Dar es salaam.