Na Victor Abuso
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF linaitaka klabu ya Simba na mshambuliaji wake Ramadhani Singano ‘Messi’ kufanya mazungumzo na kufikia mwafaka kuhusu mkataba tata wa mshambuliaji huyo.
Mshambuliaje huyo anasema kuwa mkataba wake na Simba ni wa miaka miwili na unafikia mwisho tarehe 1 mwezi Julai lakini uongozi wa Simba unadai kuwa mkataba wa mchezaji huyo ni wa miaka mitatu.
Utata umezuka kati ya pande hizi mbili kuhusu mkataba huo na tayari wamefika mbele ya uongozi wa soka nchini humo ambao umewaomba kuendelea kuzungumza ili kutatua mgogoro huo.
Kutokana na tofauti hizi, Singano ametaka kupewa Shilingi za Tanzania Milioni 50 ili asainii mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, la sivyo aangalie kwingine.
Nao uongozi wa Simba unasema upo tayari kutoa dau la Shilingi Milioni 30 ili kumaliza mzozo huu na Sindano aendelee kuichezea lakini bado mwafaka haujafikiwa.
Uamuzi huo umewasikitisha wadau, akiwamo Singano akiamini kuwa TFF ingetoa majibu sahihi ya mkataba upi kati ya ule wa Simba sanjari au ule wake, upi ulikuwa sahihi.
Hata hivyo, Singano ameonekana kutoridhika na uamuzi uliotolewa na TFF wa kumtaka akae na Simba kujadili mkataba mpya.
“Namshukuru Mungu kwa mikataba yote kuvunjwa na hiyo inamaanisha kuwa mini nipo huru lakini natoa wito kwa wachezaji wenzangu wawe makini ili haya yasiwakute,” alisema.
Wachambuzi wa soka nchini Tanzania wanasema TFF ingemaliza tofauti kati ya pande hizi mbili badala ya kuwaambia kwenda kutafuta suluhu.
“Hii inaonesha kuwa kuna jambo linalofichwa hapa katia ya TFF, Simba na mchezaji, kwanini wasingelimaliza tatizo hili ?,” Emmanuel Makundi mchambuzi wa soka jijini Dar es salaam amehoji.
Mzozo huu unazuka kipindi hiki vlabu vya soka Tanzania bara vikianza zoezi la kuwasajili wachezaji wapya kabla ya kuanza kwa msimu mpya.