Kamati ya Maadili iliyokutana Januari 18, 2018 imepitia shauri lililowasilishwa na Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF wakiwatuhumu viongozi wanne kwa makosa ya kughushi na udanganyifu wa mapato kwenye mchezo namba 94 kati ya Ndanda FC na Simba uliochezwa Disemba 30,2017.
Shauri la kwanza lililomuhusu Katibu msaidizi wa Ndanda Ndugu Selemani Kachele,Kamati imegundua kuwa mtuhumiwa aliitwa wakati wa kuhesabu mapato kuthibitisha deni dhidi ya Ndanda lenye thamani ya Shilingi Milioni mbili laki mbili na elfu hamsini(2,250,000),deni ambalo TFF waliagiza wakatwe kwenye mapato ya mechi hiyo,Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mtwara alithibitisha kuwa alimuita kuthibitisha uhalali wa deni hilo baada ya Muhasibu wa Ndanda kugoma kulipa deni hilo ambalo linahusu pango la Ndanda kwa Mama mwenye Nyumba.
Hata hivyo Kamati ilimuhoji zaidi na akashindwa kutoa uthibitisho wa kulipwa kwa deni hilo na hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa deni hilo limelipwa.
Kamati imempa onyo kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a) kanuni za maadili ya TFF toleo la 2013 na imeiomba Sekretarieti ya TFF ifuatilie kama deni hilo limeshalipwa ili kuepusha ulipaji wa Zaidi ya mara moja.
Shauri la Pili lilimuhusu Muhasibu msaidizi wa Simba Ndugu Suleiman Kahumbu.Kamati haikuendelea na tuhuma dhidi yake baada ya Sekretarieti ya TFF kuamua kuondoa shauri dhidi yake kwa kuwa alitoa ushirikiano na kutosheka kuwa hana hatia na badala yake alitumika kama shahidi wa upande wa washtaki.
Shauri la tatu lilimuhusu Katibu mkuu wa Chama cha soka Mtwara Ndugu Kizito Mbano.Kamati ilimuhoji mtuhumiwa na alikiri kuwepo kwa mawasiliano na msimamizi wa kituo Ndugu Dunstan Mkundi kuhusu nia ya kughushi fomu ya marejesho ya mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba SC.
Ndugu Kizito Mbano hakutoa taarifa yoyote ile wala kuonyesha ushirikiano kwa Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi wakati yeye akiwa msimamizi msaidizi wa kituo na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mtwara,hivyo Kamati imemkuta na hatia na imemuhukumu kutojihusisha na shughuli za Mpira wa Miguu kwa kipindi cha miaka Mitano(5) kwa mujibu wa kifungu cha 73(7) cha kanuni za maadili TFF toleo la 2013.
Shauri la nne lililosikilizwa lilikuwa la Msimamizi wa Kituo cha Mtwara Ndugu Dunstan Mkundi.Kamati baada ya kusikiliza shauri hilo imemkuta na hatia kwa kosa la kushindwa kuwasilisha fomu ya mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba ndani ya saa 48 kama kanuni inavyotaka.
Hiyo ni kinyume na Kanuni ya 32(2) Kanuni za Ligi Kuu toleo la 2015,Vilevile Kamati imemkuta na hatia ya kushindwa kusimamia mauzo ya tiketi za mchezo kati ya Ndanda FC na Simba kwa kutotoa taarifa ya tiketi zilizotumika na zile zilizobaki.
Kamati ilibaini kuwa Ndugu Dunstan Mkundi akiwa msimamizi wa kituo hakutoa ushirikiano kwa kutompa taarifa za mapato na idadi ya watazamaji Kamisaa wa mchezo Salum Singano kinyume na Kanuni ya 32(4) ya Ligi Kuu toleo la 2017.
Aidha Mkundi ambaye ni msimamizi wa kituo cha Mtwara ameshindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu utata wa fomu mbili zilizowasilishwa zilizoonyesha utofauti wa mapato kwa kiasi cha shilingi Milioni tatu laki saba kumi elfu(3,710,000).
Washtakiwa wote walihojiwa na Kamati na kuthibitisha kuwa mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba yalikuwa ni Shilingi Milioni thelathini na saba laki saba na themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni thelathini nne sabini elfu(34,070,000) ambazo Ndugu Mkundi anadai kuwa ndiyo yalikuwa mapato ya mchezo huo.
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kutoka klabu za Ndanda FC na Simba mapato ya Vilabu hivyo yalitokana na asilimia ya vyanzo kutokana na milioni thelathini na saba laki saba themanini elfu(37,780,000) na siyo Shilingi milioni thelathini nne sabini elfu(34,070,000)kama alivyowasilisha msimamizi huyo wa kituo cha Mtwara nyaraka za fedha alizoweka kwenye akaunti za TFF na Bodi ya Ligi.
Kitendo cha kughushi nyaraka na kupunguza mapato ya mchezo kati ya Ndanda FC na Simba siyo tu kimeharibu taswira ya mchezo wa Mpira wa miguu,bali pia kimepunguza mapato ya TFF,Bodi ya Ligi na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato (TRA),Baraza la Michezo la Taifa (BMT),Wamiliki wa Uwanja na Wadau wengine.
Kamati imemtia hatiani Ndugu Dunstan Mkundi kwa makosa hayo na inamfungia maisha kutojishughulisha na mchezo wa Mpira wa Miguu.
Kamati imetoa adhabu hiyo kali ili iwe fundisho kwa wale wote wanaotaka kufanya ubadhirifu wa ufisadi katika mchezo wa Mpira wa Miguu.Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF ifuatilie suala hili kwenye vyombo vya dola na mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria.
Pia Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kutafuta njia bora ya kuimarisha udhibiti wa mapato kwa kuongeza uwajibikaji wa uwazi kwa wadau wote,Vilevile Kamati inashauri Sekretarieti ya TFF na Bodi ya Ligi kuharakisha mchakato wa kukusanya mapato yake kwa njia za kielektroniki ili kuziba mianya ya upotevu.
African journalist with passion of football reporting.Also i love politics