Timu ya Simba SC imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kutoshuka Uwanjani leo baada ya wapinzani wa Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Tanzania Prisons.
Ubingwa wa Simba umepatikana baada ya wapinzani wao Yanga kufungwa mabao 2-0 na Prisons katika mchezo uliochezwa leo katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. Simba inatarajiwa kuchuana na Singida United, Jumamos katika Uwanja wa Namfua, uliopo Singida, katikati mwa Tanzania.
Simba ina alama 65 ikiwa imesaliwa na michezo mitatu wakati yanga baada ya kufungwa mchezo wa leo imesaliwa na alama 48 ikiwa na michezo minne mkononi. Hata hivyo ikiwa Yanga itashinda michezo yote iliyosalia haitaweza kufikia idadi ya alama za Simba.
Simba inatwaa ubingwa wa Tanzania baada ya kupita misimu mitano,mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa ni mwaka 2012 ilipokuwa ikinolewa na Mserbia Milovan Cirkovic.
Kwa miaka mitatu mfululizo Yanga ilitawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo sanjari na kufuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano ya taji la shirikisho Afrika mwaka 2016.
Mwandishi wa Michezo wa RFI Kiswahili, Fredrick Nwaka anasema kwa kiasi kikubwa ubingwa wa Simba umechangiwa na usajili wa wachezaji wazoefu uliofanywa na uongozi ukisaidiwa kwa kiasi kikubwa na mfanyabiashara Mohammes Dewji.
Wachezaji nyota waliosajiliwa na Simba msimu huu ni pamoja na washambuliaji Emanuel Okwi na John Bocco ambao kwa pamoja wameifungia timu yao mabao 34 kati ya mabao 60 yaliyofungwa na timu hiyo.
Yanga imeshindwa kutamba msimu huu, sababu kubwa ikitajwa ni kukosekana kwa wachezaji wake muhimu sanjari na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na kujiondoa kwa aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wa klabu hiyo Yusuph Manji.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Simba itawakilisha Tanzania Bara katika michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka 2019.