Connect with us

By Fadhili Omary Sizya

Timu ya Singida United na Mbao Fc zimekwenda suluhu 0-0 katika muendelezo wa mechi za ligi kuu Tanzania bara TPL katika uwanja wa Namfua mkoani Singida.

Timu zote zilianza kwa kasi, soka la kushambuliana kwa zamu na kandanda safi lakini hakuna timu iliyofanikiwa kuona nyavu za mpinzani wake.

Kipindi cha kwanza kilionekana kuwa na purukushani zaidi, washambuliaji Lubinda Mundia, Hans Kwofie kwa upande wa Singida na Pastory Athanas upande wa Mbao kama wangekuwa makini wangeweza kuzisaidia ushindi timu zao.

Kipindi cha pili, Singida ilikuja kasi baada ya kocha Jumanne Charles wa Singida kufanya mabadiliko kadhaa, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kucheza vyema mipira ya krosi zilizochongwa na winga wa zamani klabu ya Yanga Godfrey Mwashiuya na kumaliza suluhu dakika zote 90.

Katika takwimu za mchezo, Singida walimaliza kwa umiliki mzuri wa mpira asilimia 52 dhidi ya Mbao, huku Mbao wakitamba katika mipira iliyolenga lango wakipiga mashuti mengi dhidi ya wapinzani wao.

Baada mchezo huo Mbao Fc imecheza mechi ya tatu mfululizo bila kupoteza na kufanikiwa kukaa kileleni ligi kuu wakiwa na alama 7, huku Singida ikiambulia alama 4.

Ligi kuu itaendelea tena kesho Jumamosi kwa mechi kadhaa kuweza kuchezwa zikiondolewa mechi mbili za Azam Fc pamoja Simba kutokana na wingi wa wachezaji wa timu hizo ambao wamejiunga na kambi ya Timu ya taifa Taifa Stars inayojiandaa na mechi dhidi ya Timu ya taifa ya Uganda kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika Afcon 2019 nchini Cameroon.

 

More in