Mabingwa wa mwaka 2010 wa taji la klabu bingwa barani Afrika TP Mazembe ya DRC, siku ya Jumanne wanatarajiwa kwenda jijini Algers nchini Algeria, kuanza maandalizi ya kumenyana na MC Alger katika mchuano muhimu wa kuwania taji la msimu huu.
Maandalizi haya ya mapema yanakuja kuelekea mechi ya Jumamosi katika uwanja wa Stade du 5 Juillet jijini Algers baada ya ushindi wa nyumbani.
TP Mazembe wakiwa nyumbani mjini Lubumbashi, waliifunga MC Alger bao 1-0, lililofungwa na Elia Meschak katika dakika ya 88 ya mchuano huo uliochezwa wiki iliyopita.
Wiki mbili baadaye, Mazembe wanatarejea kurejea tena nchini humo kumenyana na Entente Sportive de Setif tarehe 17 mwezi Agosti katika mchuano mwingine muhimu wa kufuzu katika hatua ya robo fainali kutoka kundi B.
Mazembe wanaongoza kundi hilo kwa alama 9, baada ya kushinda mechi zake zote tatu.
Wenyeji wa mchuano wa wiki hii MC Alger, wana alama nne, ES Setif ina alama tatu huku Difaa El Jadida ya Morocco ni ya mwisho kwa alama moja katika kundi hilo.