Connect with us

Michuano ya soka hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika, zitapigwa mwishoni mwa wiki hii.

Kuanzia Ijumaa usiku, USM Alger ya Algeria itakuwa nyumbani kumenyana na Wydad Casablanca ya Morocco.

Wawakilishi hao wa Algeria, walifuzu katika hatua hiyo baada ya kuwaondoa Ferroviario Beira ya Msumbuji katika hatua ya robo fainali.

Wydad Casablanca nayo, iliiwashangaza mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa kuwaondoa katika hatua hiyo.

Mechi za nusu fainali zitachezwa nyumbani na ugenini.

Mchuano mwingine utachezwa siku ya Jumapili, Oktoba 1 2017 kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Al-Ahly ya Misri.

Klabu zote zilizofika katika hatua hii ni kutoka Kaskazini mwa bara la Afrika, nchini Misri, Algeria, Morocco na Tunisia.

Kuhusu michuano ya Shirikisho, mabingwa watetezi TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, watakuwa nyumbani katika uwanja wao wa Kamalondo mjini Lubumbashi kumenyana na FUS Rabat ya Morocco.

Mechi zote za Shirikisho, zitachezwa siku ya Jumapili.

TP Mazembe inashinikizo kubwa ya kushinda mechi hii ya mzunguko wa kwanza, baada ya kufuzu kwa kuishinda Al Hilal ya Sudan kwa mabao 7-1.

Wawakilishi wa Afrika Kusini, SuperSport United, watachuana na Club Africain ya Tunisia.

 

More in