Na Victor Abuso,
Mabingwa mara nne wa taji la klabu bingwa barani Afrika TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watamenyana na mabingwa wa CECAFA, Azam FC ya Tanzania katika mchuano wa kirafiki wa Kimataifa.
Mchuano huo utaisaidia Mazembe katika mechi yake ya kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika CAF dhidi ya Al Hilal ya Sudan tarehe 23 mwezi huu.
Afisa Mkuu wa klabu ya Azam, Saad Kawemba ameliambia Gazeti la The Citizen kuwa mchuano huo pia utawasaidia kwa maandalizi ya ligi kuu ya Tanzania bara mwezi ujao lakini pia mchuano wa hisani ya ngao dhidi ya Yanga tarehe 22 mwezi huu.
Mbali na TP Mazembe, Matajiri hao wa jiji la Dar es salaam wamepiga kambi visiwani Zanzibar kwa maandalizi yake lakini pia imeratibiwa kumenyana na Zesco United ya Zambia na Silver Strikes ya Malawi katika michuano mingine ya kirafiki.
Mwishoni mwa juma lililopita, Mazembe ikiwa nyumbani katika uwanja wake mjini Lubumbashi iliifunga Smouha ya Misri bao 1 kwa 0 na sasa inaongoza kundi lao kwa alama nane.
Huu ni ushindi wa pili dhidi ya klabu hii ya Misri kwa sababu mchuano wa kwanza mjini Alexandria mwezi uliopita, TP Mazembe walipata ushindi wa mabao 2 kwa 0 wakiwa ugenini.