Michuano ya nusu fainali ya pili, kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika itachezwa mwishoni mwa juma hili.
Kesho mabingwa watetezi wa taji la Shirikisho, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watakuwa ugenini kucheza na FUS Rabat ya Morocco.
Mechi ya kwanza, wiki kadhaa zilizopita, Mazembe walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi.
Siku ya Jumapili, SuperSport United ya Afrika Kuisni nayo itakuwa nchini Tunisia kucheza na Club Africain.
Mechi ya kwanza, timu zote mbili zilitoka sare ya bao 1-1.
Mshindi katika michuano hii atafuzu katika hatua fainali itakayochezwa katika mizunguko miwili mwezi Novemba.
Mambo yatakuwa hivyo katika harakati za kumtafuta bingwa wa taji la klabu bingwa, ambapo kesho Wydad Casablanca ya Morocco itakuwa nyumbani kumenyana na USM Alger ya Algeria.
Nusu fainali ya kwanza, vlabu vyote viwili havikufungana.
Mabingwa wa zamani wa taji hili Al-Ahly, nao watakuwa katika uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria siku ya Jumapili kukabiliana na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Mechi ya kwanza, Etoile du Sahel, ilipata ushindi wa mabao 2-1.
Fainali ya kwanza, itachezwa mwishoni mwa mwezi huu huku ile ya kwisho ikipigwa mapema mwezi Novemba.