Klabu ya TP Mazembe nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao ni mabingwa watetezi wa taji la Shirikisho barani Afrika, watamenyana na Recretivo do Libolo ya Angola katika michuano ya hatua ya robo fainali itakayoanza mwezi Septemba.
Mazembe itaanza harakati zake ugenini kati ya tarehe 8 na 10 mwezi Septemba huku mchuano wa marudiano ukichezwa kati ya tarehe 15-17 mwezi huo.
Mshindi baada ya mechi zote mbili, atafuzu katika hatua ya nusu fainali.
FUS Rabat ya Morocco, itakabiliana na CS Sfaxien ya Algeria huku SuperSport United ikipangwa na ZESCO United ya Zambia.
MC Alger ya Algeria itakabiliana na Club Africain ya Tunisia.
Nao, mabingwa watetezi wa taji la klabu bingwa barani Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, itamenyana na Wydad Casablanca ya Morocco.
Wawakilishi wa Msumbiji Ferroviario Beira watapambana na US Alger ya Algeria huku Al-Ahly ya Misri ikichuana na Esperance de Tunis ya Tunisia.
Al-Ahli Tripoli ya Libya itacheza na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Michuano hii ya klabu bingwa na Shirikisho imetawaliwa na vlabu kutoka nchini Tunisia, Etoile du Sahel, Esperance de Tunis (Michuano ya klabu bingwa) huku CS Sfaxien na Club Africain zikiwakilisha nchi hiyo katika michuano ya Shirikisho.