Klabu ya soka ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itamenyana na USM Alger ya Algeria katika fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika CAF.
Mazembe walifuzu katika hiyo baada ya kuwafunga Al Merrikh ya Sudan mabao 3 kwa 0 katika mchuano muhimu wa marudiano wa nusu fainali uliochezwa mwishoni mwa juma jijini Lubumbashi.
Mchuano wa kwanza wa nusu fainali walifungwa mabao 2 kwa 1 jijini Khartoum.
Mshambuliaji wa Kimataifa kutoka nchini Tanzania Mbwana Samatta aliifungia klabu yake mabao 2 katika kipindi cha pili cha mchuano huo.
Hadi sasa Samatta ameifungia klabu yake mabao 6 katika michuano hii ya klabu bingwa lakini aliyekuwa anayeongoza ni Bakri Al-Madina wa Al-Merrikh kwa magoli 7.
USM Alger nayo ilifuzu baada ya kuishinda klabu nyingine ya Sudan Al Hilal kwa mabao 2 kwa 1.
Mchuano wa nusu fainali ya pili vlabu hivyo viwili vilitoka sare ya kutofungana jijini Algeria.
Wachambuzi wa soka walikuwa wametabiri kuwa TP Mazembe na USM Alger wangekutana katika fainali itakayochezwa mapema mwezi wa Novemba nyumbani na ugenini.
Mbali na michuano ya klabu bingwa, Orlando Pirates ya Afrika Kusini itachuana na Etoile du Sahel ya Tunisia katika fainali ya kuwania taji la Shirikisho.
Orlando Pirates waliwafunga Al Ahly ya Misri mabao 4 kwa 3 katika mchuano wa mzunguko wa pili wa nusu fainali huku Etoile du Sahel wakifuzu kwa jumla ya mabao 5 kwa 4 baada ya kuwashinda Zamalek.