Klabu ya soka ya TP Mazembe imeondolewa katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kulemewa na Wydad Casablanca ya Morocco baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 katika mchuano wa marudiano Jumatano jioni.
Matokeo haya yanamaanisha kuwa Wydad Casablanca imefuzu katika hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 3 kwa 1 baada ya ushindi wa mabao 2 kwa 0 katika mchuano wa kwanza wiki moja iliyopita.
Mashabiki wa TP Mazembe walikuwa na matumaini makubwa baada ya Salif Coulibaly kuwapa raha na matumaini kwa kuipa timu yake bao la ufunguzi katika dakika ya 28 kipindi cha kwanza.
Mazembe ambao walioneakana kucheza kwa kujituma mbele ya mashabiki wake, walishindwa kupita ngome ngumu ya wapinzani wao kipindi chote cha pili.
Mambo yalibadilika na yakawa mabaya zaidi katika dakika ya mwisho ya 90 baada ya Reda El Hajaoui kuisawazishia timu yake na hivyo kuyafanya matokeo hayo kuwa bao 1 kwa 1 hadi kipenga cha mwisho.
Mashabiki wa Mazembe waliofika kushuhudia mchuano huu wamerudi nyumbani wakiwa wamevunjika mioyo lakini hawajakata tamaa kwa sababu klabu yao sasa itacheza katika hatua ya mwondoano kutafuta taji la Shirikisho.
TP Mazembe wameondoka katika michuano hii baada ya kuweka rekodi ya kushinda mataji 5 mwaka 1967, 1968,2009,2010 na 2015.