Tusker FC inahitaji ushindi mmoja kuthibitishwa kuwa mabingwa wa ligi kuu ya soka nchini Kenya msimu huu.
Siku ya Jumapili, Tusker itakuwa nyumbani kupambana na AFC Leopards katika mchuano muhimu kuelekea kumalizika kwa ligi kuu tarehe 19 mwezi Novemba.
Baada ya kuchezwa kwa mechi 28 msimu huu, Tusker inaongoza msururu wa ligi kwa alama 55 ikifuatwa na Gor Mahia ambayo ina alama 51.
Mchuano ujao wa Gor Mahia utakuwa siku ya Alhamisi, na ikiwa itapata ushindi na Tusker kupoteza mchuano wake siku ya Jumapili, itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kushinda ligi.
Mchuano wa mwisho utakuwa kati ya mabingwa hao watetezi na Tusker FC katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi tarehe 19 mwezi Novemba.
Mbali na michuano hiyo, John Makwatta anaongoza katika safu ya ufungaji wa mabao baada ya kuifungia klabu yake ya Ulinzi Stars mabao 13.
Wycliffe Ochomo wa Muhoroni Youth na Kepha Aswani anayechezea AFC Leopards wamefunga mabao 12 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Jacques Tuyisenge aliyeifungia klabu ya Gor Mahia mabao 9.