Rwanda, imeonesha mfano mzuri katika ukada wa nchi za Maziwa makuu kwa kufanikisha uwenyeji wa mashindano ya kufana ya CHAN, kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walinyakua ubingwa baada ya kuifunga Mali mabao 3 kwa 0 katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali, na kuweka historia kuwa taifa la kwanza kunyakua taji hili mara mbili baada ya kufanya hivyo mwaka 2009.
Baada ya Rwanda, Kenya imepewa kijiti cha kuwa mwenyeji wa mashindano haya mwaka 2018.
Lakini je, Kenya itafanikiwa au nafasi hii itawaponyoka tena ?
Mwaka 1996, Kenya ilipewa nafasi ya kuandaa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika, lakini haikufanikiwa kwa sababu kutokuwepo kwa maandalizi mazuri lakini pia kuwepo kwa siasa kwenye mchezo wa soka.
Serikali ya Kenya imekuwa ikiahidi kuwa itajenga viwanja wa kisasa katika Kaunti zote 47 nchini humo, lakini hili halijatekelezwa kufikia sasa.
Ukarabati wa viwanja.
Rwanda ilikuwa na viwanja vinne vilivyotumiwa kuandaa mashindano haya. Uwanja wa Amahoro, Nyamirambo zote zikiwa jijini Kigali, Umuganda mjini Gisenyi na uwanja wa Huye mjini Butare.
Kenya inajivunia viwanja viwili tu vya kisasa, ule wa Moi Kasarani wenye uwezo wa kuwa na mashabiki 60,000 na ule wa Nyayo wenye uwezo wa kuwakaribisha mashabiki 30,000 vyote hivyo vipo jijini Nairobi.
Uwanja wa Moi mjini Kisumu umekuwa ukikarabatiwa lakini bado haujamalizika, hadi sasa hakuna eneo la mashabiki kuketi huku muda ukiyoyoma.
Mjini, Mombasa hali ni sawa na huko Kisumu uwanja huo bado hauna uwezo wa kuandaa mashindano ya kimataifa.
Unapotazama hili unapata kigugumizi ikiwa kweli Kenya itafanikiwa kuwa wenyeji wa CHAN mwaka 2018.
Siasa za soka.
Soka la Kenya limekuwa likiathiriwa na siasa za mara kwa mara hasa kuhusu ni nani wa kusimamia mchezo huu nchini humo.
Uchaguzi mpya wa viongozi mpya umepangwa kufanyika siku ya Jumatano Februaru 10. Je, utakuja na mafanikio kusaidia kufanikisha maandalizi ya mashindano haya ?.
Mashabiki kwenda uwanjani
Kenya imekuwa na rekodi mbaya ya mashabiki wake kutokuwa na tabia ya kufika uwanjani kushuhudia hata michuano za ligi kuu KPL.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA, Nicholas Musonye wakati mmoja alinukuliwa akisema Wakenya hawapendi kwenda uwanjani, kama jirani zao Tanzania, Ethiopia na Uganda.
Mwaka 2013 idadi ndogo ya mashabiki ilijitokeza kushuhudia michuano ya CECAFA iliyofanyika jijini Nairobi.
Sababu kuwa ya mashabiki kutoenda uwanjani ni kwa sababu ya wengi wao kupendelea ligi za barani Ulaya, badala ya zile za nyumbani.
Maandalizi ya mapema.
Rwanda ilianza kujiandaa kwa michuano ya CHAN ya mwaka 2016 mwaka 2014, Kenya inastahili kuiga mfano huu na kwa msaada wa serikali na Shirikisho la soka kutenga bajeti ya kuvikarabati vipya viwanja vya Kisumu na Mombasa kwa wakati.
Ikiwa Kenya haitafanikiwa kuanza maandalizi ya mapema na kuonekana kuwa haiweza kuwa mwenyeji, Ethiopia imetengwa kuwa mbadala wa wenyeji wa michuano hiyo.