Klabu bingwa.
AS Vita Club ya DRC, Al-Merrikh ya Sudan na Yanga FC ya Tanzania ni vlabu kutoka Afrika Mashariki na Kati vilivyopata ushindi katika michuano ya duru ya kwanza ya mzunguko wa kwanza kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika.
Vita Club ikicheza nyumbani, iliifunga Ferroviario Maputo ya Msumbuji bao 1 kwa 0, matokeo ambayo ni mazuri kwa vijana wa Florent Ibenge kuelekea mzunguko wa pili siku ya Jumapili.
Al-Merrikh nao wakicheza ugenini nchini Nigeria, walipata ushindi muhimu kwa bao 1 kwa 0 dhidi ya Warri Wolves.
Matokeo haya yanaamanisha kuwa Al-Merrikh watakuwa wanatafuta sare watakapokuwa wenyeji katika mzunguko wa pili jijini Khartoum siku ya Jumamosi.
Warri Wolves, wanastahili kupata ushindi wa mabao 2 kwa 0 ili kujihakikishia nafasi ya kusonge mbele.
Yanga FC walipata ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidi ya APR jijini Kigali, na mchuano wa marudiano utapigwa mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es salaam.
APR inastahili kushinda mabao 2 kwa 0 ili kujihakikishia kusonga mbele lakini ikipata ushindi wa bao 1 kwa 0, mchuano huo utaenda katika muda wa ziada kwa sababu timu zote mbili zitakuwa na sare ya mabao 2 kwa 2.
Matokeo mengine, St.George ya Ethiopia ikiwa nyumbani ilitoka sare ya mabao 2 kwa 2 na mabingwa watetezi TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mchuano wa marudiano ni siku ya Jumapili mjini Lubumbashi na kila klabu inaweza kushinda katika mchuano huo wa marudiano.
Kocha Hubert Velud amesema aliridhishwa na matokeo hayo lakini akasitika namna Mazembe ilivyoruhusu kufungwa mabao 2 baada ya kutangulia kupata mabao.
Vital’o ya Burundi, ilipoteza mchuano wake dhidi ya Enyimba ya Nigeria kwa mabao 5 kwa 1 huku Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mabao 2 kwa 0 AC Leopards ya Congo Brazaville.
Taji la Shirikisho
Azam FC ya Tanzania, Zanaco ya Zambia, FC Saint-Eloi Lipopo ya DRC na Sports Club Villa zilipata ushindi katika michuano yao mwishoni mwa juma lililopita.
Azam FC ikicheza ugenini nchini Afrika Kusini dhidi ya Bidvest Wits, ilipata ushindi wa mabao 3 kwa 0 na mchuano wa marudiano utachezwa siku ya Jumapili jijini Dar es salaam.
Zanaco nao wakicheza ugenini jijini Harare nchini Zimbabwe, iliishinda Harare City mabao 2 kwa 1.
FC Saint-Eloi Lupopo ikicheza nyumbani iliishinda Al-Ahly Shendi ya Sudan kwa mabao 2 kwa 1.
Matokeo mengine, Vita Club Mokanda ya Congo Brazavile ilitoka sare ya kutofunga na Police FC ya Rwanda, huku Sport Club Villa ya Uganda ikipata ushindi mkubwa wa mabao 4 kwa 0 dhidi ya JKU ya Zanzibar jijini Kampala.
Misr El-Makasa ya Misri ikiwa nyumbani, ilipata ushindi dhidi ya CS Don Bosco ya DRC wa mabao 3 kwa 1.
Washindi wa mzunguko wa kwanza watafuzu katika hatua ya mzunguko wa pili, michuano itakayochezwa mapema na baadaye mwezi Aprili.