Na: Victor Abuso
Fainali ya makala ya mwaka 2015 kuwania taji la soka baina ya vlabu vya Afrika Mashariki na Kati CECAFA au taji la Kagame inachezwa leo Jumapili katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam nchini Tanzania kuanzia saa 10 jioni saa za Afrika Mashariki.
Gor Mahia ya Kenya ambayo mwisho ilinyakua taji hili mwaka 1985 wakati walipowashinda ndugu zao na watani wao wa jadi AFC Leopards katika fainali iliyochezwa nchini Sudan.
Azam FC ya Tanzania iliyozinduliwa mwaka 2007 ilifika fainali ya kwanza ya michuano hii ya CECAFA mwaka 2012 na kukutana na Yanga FC pia ya Tanzania na kufungwa mabao 2 kwa 0 wakati michuano hiyo ilipofanyika jijini Dar es salaam.
Gor Mahia na Azam FC ziliongoza makundi yao kuelekea fainali ya michuano hii.
Gor Mahia ikitoka sare mchuano mmoja huku Azam ikihakikisha kuwa haifungwi bao lolote katika muda wa kawaida ukiondoa mabao 3 waliofungwa wakati wa mikwaju ya penalti dhidi ya Yanga katika hatua ya robo fainali.
Wachezaji wa kuangaliwa kwa upande wa Gor Mahia ni pamoja na mshambuliaji Michael Olunga ambaye ameifungia klabu yake mabao 5 katika michuano hii na anaongoza kuwa mfungaji bora kuelekea fainali.
Olunga anafahamika kwa kasi aliyonayo akishirikiana kwa karibu na washambuliaji Meddie Kagere kutoka Uganda pamoja na Godfrey Walusimbi.
Kocha wa Gor Mahia Mwingereza Frank Nuttal pia anajivunia wachezaji kama Karim Nigiziyimana, Aucho Khalid,Collins Okoth na nahodha Musa Muhammad.
Klabu ya Azam ambayo inajivunia kuwasajili wachezaji kwa kiasi kikubwa cha fedha inajivunia wachezaji kama Nahodha John Bocco, Aggrey Morris, mshambuliaji matata Kipre Tchetche kutoka Cote D’ivoire ambaye amekuwa akisumbua ngome za timu mbalimbali katika michuano hii.
Jean Baptiste Mugiraneza raia huyu wa Rwanda, ni kiungo wa kati ambaye anategemewa sana katika mchuano huu wa fainali kutoa pasi kwa wenzake huku beki Pascal Serge Wawa raia wa Cote Dvoire ambaye ameonekana mwamba katika beki ya klabu yake na kuwazuia washambuliaji kutikisa nyavu akitarajiwa kutumia uzoefu na misuli yake kuwazuia washambuliaji kutopita ukuta wa Azam.
Ni fainali ya kukata na shoka, mchuano mgumu na utakaojaa msisimko mkubwa na wachezaji wa pande zote mbili wakitunishana misuli katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.