Timu ya taifa ya soka ya Uganda, itamenyana na Madagascar siku ya Jumatano katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki kabla ya kumenyana na Ghana katika mchuano muhimu wa kufuzu kucheza kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Lugogo jijini Kampala, kuanzia saa 10 jioni saa za Afrika Mashariki.
Kocha Moses Basena amesema mchuano huu ni muhimu kwa sababu utasaidia kikosi chake kujiweka tayari kuikabili Black Stars, siku ya Jumamosi.
Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Namboole jijini Kampala.
Uganda wanakwenda katika mechi hii wakiwa katika nafasi ya pili katika kundi E kwa alama 7, nyuma ya Misri ambao wana alama 9 baada ya kucheza michuano minne kila mmoja.
Ghana, ambao wameshinda mchuano mmoja hadi sasa katika kundi hili wana alama 5, katika nafasi ya tatu.
Mchuano wa kwanza mataifa mawili hayakufungana wakati Ghana walipokuwa wenyeji mjini Tamale.