Timu ya taifa ya soka ya Uganda imenyakua ubingwa wa mwwaka 201 wa taji la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA.
Uganda Cranes walitawazwa mabingwa baada ya kuishinda Amavubi Stars ya Rwanda katika fainali iliyopigwa Jumamosi jioni katika uwanja wa Taifa jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Bao la ushindi la Uganda lilitiwa kimyani na Caesar Okhuti katika dakika ya 15 ya mchuano huo kupitia mkwaju wa kichwa.
Hili ni taji la 14 kwa Uganda kunyakua katika historia ya mashindano haya ya CECAFA .
Mshambuliaji wa Uganda Farouk Miya ambaye amekuwa akiifungia timu yake mabao katika michuano mbalimbali, alikosa nafasi nyingi za kuipa Uganda mabao zaidi katika mchuano kutokana na mashuti yake kutoka nje.
Rwanda walionekana kuimarika kipindi cha pili kwa kuutawala mchezo na jitihada za wachezaji kama Jean Baptiste Mugiraneza na Jacques Tusiyesenge kupata mabao ziliambua patupu kutokana na uimara wa beki ya Uganda hasa kipa Ismail Watenga.
Pamoja na kushinda taji hili, historia inaonesha kuwa Uganda wamefika katika fainali 18 katika mashindano haya ya CECAFA, kushinda 14 na kufungwa 4.
Huu ni ushindi wa kwanza wa kocha Milutin Micho ambaye amekuwa akiifunga Cranes kwa miaka mitatu sasa.
Mwaka 2011 wakati michuano ya CECAFA ilipofanyika nchini Tanzania, Uganda pia waliwashinda Rwanda katika hatua ya fainali wakati huo Micho akiwa kocha wa Amavubi Stars.
Rwanda imewahi kushinda taji la CECAFA mara moja tu mwaka 1999, walipowafunga Kenya mabao 3 kwa 1.
Wenyeji wa mashindano haya Ethiopia, walimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Sudan mabao 5 kwa 4 kupitia mikwaju ya penalti baada ya mchuano huo kumalizika kwa sare ya bao 1 kwa 1.