Shirikisho la soka duniani FIFA limetangaza orodha ya mataifa bora duniani katika mchezo wa soka kwa mwezi uliopita wa Julai.
Duniani, timu ya taifa ya Argentina inaendelea kuongoza ikifuatwa na Ubelgiji.
Colombia ni ya tatu, huku Ujerumani ikifunga nne bora.
Barani Afrika, Algeria imeendelea kuongoza huku ikishikilia nafasi ya 32 duniani.
Ghana ni ya pili lakini ya 35 duniani, huku Ivory Coast ikiwa ya tatu na ya 36 duniani.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni ya tisa barani Afrika na 56 barani Afrika na imepanda nafasi tatu.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Uganda kwa mara nyingine imeendelea kuongoza lakini ni ya 65 duniani baada ya kupanda nafasi nne.
Kenya ni ya pili katika ukanda huo na ya 88 duniani, na imeshuka nafasi mbili kutoka nafasi ya 86 iliyokuwa mwezi wa Juni.
Rwanda imeshuka nafasi 10 na sasa ni ya 121 duniani na ya tatu katika ukanda, huku Burundi ikishikilia nafasi ya nne na ya 123 duniani baada ya kupanda nafasi mbili.
Tanzania imeshuka nafasi moja hadi katika nafasi ya 124 na ni ya tano katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ethiopia ni ya sita lakini ya 130 duniani baada ya kupanda nafasi mbili.
Duniani, Sudan ni ya 141 huku Sudan Kuisni ikiwa ya 153.