Connect with us

Uganda Cranes imeyaaga mashindano ya kutafuta bingwa soka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN, wakiwa na alama moja baada ya kutofungana na Ivory Coast siku ya Jumatatu.

Mchuano huo ulichezwa katika uwanja wa Marrakech, nchini Morocco ambao ndio wenyeji wa mashindano haya.

Uganda inarejea nyumbani jijini Kampala, baada ya kushindwa michuano miwili na kutofungana mchuano mmoja.

Wawakilishi hawa wa Afrika Mashariki walianza vibaya baada ya kufungwa na Zambia mabao 3-1 lakini Namibia wakawalemea kwa bao 1-0.

Kocha Sébastien Desabre raia wa Ufaransa alipewa kazi ya kuifunza Uganda wiki kadhaa kabla ya michuano hii mikubwa barani Afrika na chama cha soka nchini Uganda, kimewataka mashabiki kuwa na uvumilivu.

Uganda wameendeleza rekodi mbaya katika michuano tangu ilipoanza kushiriki mwaka 2011, 2014, 2016 na sasa mwaka 2018 ambako imeondolewa katika hatua ya makundi katika michuano hiyo yote.

Zambia na Namibia ambazo zimefuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano hii kutoka kundi B, kwa alama saba, zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchuano wao wa mwisho.

Siku ya Jumanne, michuano ya kundi C, zinatamatishwa kwa mechi zote kuchezwa kwa wakati mmoja katika uwanja wa Adrar mjini Agadir.

Rwanda ambayo ina alama nne katika kundi hii, inahitaji ushindi au sare dhidi ya Libya ili kufuzu katka hatua ya robo fainali.

Nigeria wapo katika nafasi nzuri pia wakiwa na alama nne, na itamenyana na Equitorial Guinea katika mchuano wake wa mwisho.

Ratiba ya Jumatano usiku:-Kundi D

Congo v Angola

Burkina Faso v Cameroon

Michuano ya robo fainali inachezwa siku ya Jumamosi na Jumapili.

Morocco itacheza na Namibia, huku Zambia ikicheza na Sudan.

 

More in