Na Victor Abuso,
Klabu ya soka ya Lweza FC nchini Uganda, ina siku mbili kukata rufaa dhidi ya hatua ya Shirikisho la soka nchini humo kuwashusha daraja.
Kamati ya FUFA, inasema kuwa klabu hiyo kutoka mitaa ya Kajjansi imeshindwa kutimiza masharti ya kuendelea kushiriki katika ligi kuu msimu huu licha ya kusalia katika ligi hiyo msimu uliopita.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bernard Ogwel amesema uongozi wa Lweza FC umeshindwa kuthibitisha umiliki wa uwanja wao, mikataba ya wachezaji, viongozi wa klabu hiyo na kocha wake.
Ogwel amesisitiza kuwa kwa sababu klabu hiyo iliyoshiriki ligi kuu msimu uliopita, haijatekelaza masharti hayo, imeshushwa daraja.
Hata hivyo, msemaji wa klabu hiyo Abdul Suleiman Semugenyi amesema klabu yake itatekeleza masharti hayo yote kabla siku ya Ijumaa wiki hii.
Masaibu ya klabu hii iliyozinduliwa mwaka 1990 katika mtaa wa Kajjansi jijini Kampala, yanakuja baada ya kutangazwa mabingwa wa taji la Vipers mwaka 2015.