Ujumbe wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, ukiongozwa na Naibu rais Kabele Camara na Katibu Mkuu Hicham Amrani utazuru nchini Kenya mapema wiki ijayo kuthathmini utayari wa nchi hiyo kuandaa michuano ya bara Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN mwezi Januari mwaka 2018.
Ziara hii inakuja wakati huu kukiwa na mashaka ya Kenya kuandaa michuano hii kwa sababu ya maandalizi mabaya yanayoshudiwa baada ya kupewa nafasi hiyo baada ya Rwanda kufanikiwa kuwa mwenyeji mwaka 2016.
Changamoto kubwa inayokabili Kenya ni ukosefu wa viwanja vya Michezo kwa mujibu wa kanuni za CAF.
Kuandaa fainali za CHAN, mwenyeji anastahili kuwa na viwanja vinne katika miji mbalimbali nchini humo.
enya ina viwanja viwili tu, vinavyoonekana kukamilika ule wa Kimataifa wa Kasarani na Nyayo vyote ambavyo vipo katika jiji kuu Nairobi.
Hadi sasa CAF, inasema uwanja wa Kasarani ndio ulio katika nafasi nzuri ya kuandaa michuano hiyo.
Tayari serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Michezo, imetangaza Kamati andalizi ya michuano hii ikiongozwa na rais wa Shirikisho la soka FKF Nick Mwendwa.
Mwendwa mwenyewe amenukuliwa akisema kuwa, uhaba wa viwanja nchini humo huenda ukakwamisha Kenya kuandaa fainali hii.
Ripoti zinasema kuwa ikiwa Kenya itaonekana kutokuwa tayari, Ethiopia au Morocco huenda zikapewa nafasi hiyo.