Ujumbe wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, unazuru Kenya kwa muda wa siku sita zijazo kuthathmini utayari wa nchi hiyo kuwa wenyeji wa michuano ya CHAN mwezi Januari waka 2018.
Maafisa hao wa CAF wanazuru viwanja vitakavyotumiwa kuandaa michuano hiyo inayowahusisha wachezaji wanaocheza soka barani Afrika.
Mbali na viwanja, hoteli zitakazowahifadhi wageni na hospitali za kutoka huduma muhimu za kiafya pia ni baadhi ya maeneo ambayo ujumbe huo utazuru.
Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi, pamoja na ule wa Nyayo, vinatarajiwa kutumiwa katika michuano hiyo.
Uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret na Kinoru mjini Meru, zinakarabatiwa kuwa tayari kwa michuano hii.
Ujumbe huo pia utakutana na Naibu rais William Ruto baadaye wiki hii ili kupata hakikisho la serikali kuwa michuano hii itaendelea.