Timu ya taifa ya soka ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Gabon , Morroco na Guinea zimefuzu katika hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kufuzu katika kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Uganda Cranes walifuzu kwa jumla ya mabao 4 kwa 0 baada ya kuishinda Togo nyumbani na ugenini.
Mapema juma lililopita, Uganda walipata ushindi wa bao 1 kwa 0 mjini Lome, na baadaye kupata ushindi mkubwa wa mabao 3 kwa 0 nyumbani jijini Kampala huku mshambuliaji Farouk Maya akifunga mabao mawili .
Jamhuri ya Kideokrasia ya Congo maarufu kama Leopard nayo ilitoka sare ya mabao 2 kwa 2 na Burundi jijini Kinshasa baada ya kupata ushindi wa mabao 3 kwa 2 jijini Bujumbura.
Zambia waliishinda nyumbani na ugenini Sudan baada ya kuwafunga mabao 2 kwa 0 nyumbani na bao 1 kwa 0 ugenini.
Michuano hii inaendelea siku ya Jumanne.
Kenya watapambana na Cape Verde, Tanzania na Algeria huku Rwanda wakiwakaribisha Libya jijini Kigali.
Mataifa 20 yanatarajiwa kufuzu katika hatua ya makundi na mshindi katika kila kundi atafuzu katika michuano ya dunia.