Connect with us

Wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Afrika Kusini wametia saini mkataba wa kuzingatia nidhamu kuelekea mchuano muhimu wa kufuzu kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Kocha Stuart Baxter amesema umuhimu wa mkataba huo ni kuwasaidia wachezaji kuepuka kujihusisha na tabia zisizofaa kama kujiburudisha kupita kiasi kama ilivyokuwa katika mchuano muhimu dhidi ya Cape Verde mwezi Septemba.

Mechi hiyo ilichezwa mjini Durban na Bafana Bafana kufungwa mabao 2-1, matokeo ambayo yaliwakera mashabiki wa soka nchini humo.

Inaaminiwa kuwa, hatua ya wachezaji kujihusisha katika burudani ya muda mrefu ya kunywa pombe kabla ya mchuano huo, ulichangia pakubwa wao kufungwa.

Kocha Baxter amesema hatua hii imechukuliwa kuwaonesha wachezaji hao kuwa, wao ni watalaam wanaocheza soka.

Wachezaji wa Afrika Kusini wanajiandaa kumenyana na Burkina Faso siku ya Jumamosi katika uwanja wa Soccer City, jijini Johannesburg.

Afrika Kusini ambayo ni ya mwisho katika kundi D kwa alama moja, bado ina uwezo wa kufuzu katika michuano hiyo iwapo itashinda mechi ya Jumamosi, lakini pia kuilemea Senegal nyumbani na ugenini.

Kundi hili linaoongozwa na Burkina Faso kwa alama sita baada ya mechi nne, huku Cape Verde itakayomenyana na Senegal ikiwa ya pili kwa alama sita.

Senegal ni ya tatu kwa alama 5 baada ya mechi tatu.

More in