Uwanja wa Taifa wa Tanzania uliopo Dar es Salaam utaanza kutumika tena Novemba 21 baada ya kukamilika kwa matengenezo yaliyodumu kwa miezi mitatu.
Uwanja huo unaoingiza watazamaji 60000 ulifungwa kwa muda ili kupisha matengenezo ikiwemo sehemu ya kuchezea, na maeneo mengine.
Waziri wa Habari wa Serikali ya Tanzania Dr Harrison Mwakyembe ameomba kuandaliwa kwa mchezo wa kirafiki kati ya Novemba 24, 25 au 26 ili kuufungua rasmi mchezo huo.
Akipokea ripoti hiyo kutoka kwa Alex – Mtaalamu kutoka Uingereza, Mheshimiwa Waziri Dk. Mwakyembe amesema: “Tuna changamoto kwenye matunzo na matengenezo. Sasa ili kukabiliana na changamoto hii, hatuna budi vijana sita waliofundishwa kazi na mtaalamu huyu, wakafanyiwa mpango wa ajira. Vijana hao wavumilie kwa sasa”
Mtaalamu huyo wa Uingereza, amesema kwamba wakati uwanja unatumika, ukarabati wa mara kwa mara utakuwa ukiendelea ili kuifanya hazina hiyo ya taifa kuendelea kuboreka kwa wakati wote.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumzia uboreshaji huo, alisema: “Ni vema wataalamu hao wakatumike pia kwenye viwanja vya mikoani. Huko wataviboresha na kuwafundisha wengine.”