Na Victor Abuso,
Klabu ya soka ya Vipers ina asilimia 100 ya kunyakua ubingwa wa ligi kuu ya soka nchini Uganda msimu huu baada ya kushinda mchuano wake muhimu mwishoni mwa juma hili kwa kuwafunga mabingwa mara 16 Sports Club Villa mabao 2 kwa 0 katika uwanja wa Nakivubo jijini Kampala.
Mabao hayo muhimu ya Vipers yalitiwa kimyani na Deus Bukenya katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo huku Keziron Kizito akifunga la pili katika kipindi cha pili katika mchuano huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki.
Ushindi wa Vipers unawapa uongozi wa ligi hiyo kwa alama 66 huku SC Villa ikiwa ya pili kwa alama 62.
Vipers wana mkono mmoja kwenye taji la msimu huu na sasa wanasubiri mchuano wao wa mwisho dhidi ya klabu ya BUL FC juma lijalo ili kujihakikishia ubingwa wa msimu huu licha ya SC Villa kuwa na rufaa ya kulalamikia mmoja wa mchuano wake.
Mara ya mwisho kwa Vipers kunyakua ubingwa nchini Uganda ilikuwa ni mwwaka 2010 wakati huo klabu hiyo ikifahamika kama Bunnamwaya FC.
Katika matokeo mengine ya michuano ya ligi hiyo inayofikia ukingoni, mabingwa watetezi Kampala City Council (KCC) waliendelea kufanya vibaya msimu huu baada ya kufungwa na Soana mabao 2 kwa 1 katika uwanja wa Kavumba.
Uwanjani Lugazi, Uganda Revenue Authority (URA) waliwanyuka Police FC mabao 2 kwa 1 huku BUL FC wakitoka sare ya kutofungana na Express FC mjini Jinja.
Tayari vlabu vya Entebbe FC na Rwenshama FC vimeshushwa daraja msimu huu na sasa kazi kubwa ni kwa Kira Young FC, Soana, Lweza na Simba kuhakikisha kuwa zinashinda michuano ya mwisho ili kuepuka kushushwa daraja
Michuano ya mwisho itapigwa siku ya Jumanne juma lijalo katika viwanja mbalimbali nchini Uganda, ambako michuano inayosubiriwa kwa hamu kubwa ni kati ya mabingwa watarajiwa Vipers FC dhidi ya BUL FC, Lweza FC dhidi ya KCC, Kira Young FC nayo itapambana na Simba FC.
Mecho zote zitapigwa kuanzia saa 10 na nusu jioni saa za Afrika Mashariki.