Mabingwa wa soka nchini Yanga leo usiku wanaanza kampeni ya kuwania taji la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria. Huo utakuwa mchezo wa kwanza wa Kundi D kwa Yanga ambayo imefuzu kucheza hatua ya makundi kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu.
Mchezo huo utaanza saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki sawa na saa tano usiku kwa saa za Afrika ya Kati.
Yanga ilisafiri kwenda Algeria bila kuwa na wachezaji watano wa kigeni ambao wameshindwa kusafiri kwa sababu mbalimbali ikiwemo majeraha.
Wachezaji hao ni Thaban Kamusoko na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, Papy Kabamba Shishimbi kutoka DRC, Obrey Chirwa kutoka Zambia.
Wachezaji wengine ambao wameshindwa kuambatana na Yanga katika mchuano huo ni Kelvin Yondan, Ibrahim Ajibu na Nadir Haroub Cannavaro.
Mchezo mwingine wa Kundi D utakuwa baina ya Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Amahoro, Jijini Kigali.