Yanga na Simba zinaongoza kwa kuchuana katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku zikiwa zimesalia mechi tisa ligi kumalizika.
Simba inakaa kileleni ikiwa na alama 49 wakati wapinzani wao yanga wana alama 46 katika nafasi ya pili na zote zimecheza mechi 21. Azam iko nafasiya tatu ikiwa na alama 44 na inaweza kuchupa hadi nafasi ya pili ikiwa itaiadhibu Mbeya City katika mchezo utakaochezwa Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Simba itakuwa na kibarua kizito cha kulinda uongozi wake itakapocheza na Mtibwa Sugar Jumatatu katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro. Jana Mtibwa Sugar iliichapa Singida United mabao 3-0 na kufikisha alama 30.
Yanga haitakuwa na mchezo wikendi hii kwa sababu inakabiliwa na kibarua cha kuchuana na Welatya Dicha katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika.
Timu za Mbao FC, Njombe Mji na Majimaji zinachuana mkiani mwa ligi kuu ambapo timu mbili za mwisho zitateremshwa daraja.