#Makala: Yanga ‘wameisaidia‘ Simba au ‘wameiangamiza‘ katika usajili wa kina Kagere?
Oktoba 10, mshambulizi Mnyarwanda, Meddie Kagere atafikisha miaka 32. Kwa mwanasoka si umri mbaya- kwani ni wakati ambao uzoefu, mbinu na maarifa huwa ‘mwongozo‘ wa matarajio bora.
Meddie amesajiliwa Simba SC na kutambulishwa rasmi wiki hii. Ameondoka Gor Mahia FC akiwa mshindi wa mataji matatu ya ligi kuu Kenya ( SportPesa Premier League), Kagere ameshinda pia vikombe vya FA na SportPesa Super Cup katika miaka yake miaka Gor.
Huyu ni mchezaji ambaye anasubiri timu yake icheze vizuri, kumiliki mchezo na viungo wampigie pasi za mwisho. Huyu ni mmaliziaji wa kiwango cha juu- hakuna ubishi, lakini alipaswa kwenda kuisaidia Yanga SC ama kuendelea kubaki Gor na si Simba ambao ‘wanajinadi‘ wanaweza kusaini mwanasoka yeyote ndani ya Afrika.
Mlinzi wa kati, Muivory Coast, Serge Paschal Wawa, golikipa wa zamani wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida‘ nao kama ilivyokuwa kwa Adam Salamba, Marcel Kaheza, Mohamed Rashid na Kagere nao wamemsaini kuichezea Simba mara baada ya kuripotiwa kuhitajika kwanza Yanga.
‘Ni usajili wa kukomoana‘ tu, kwasababu kama Kweli Simba wana mtazamo wa mbali walipaswa wao wenyewe kutazama mapungufu yao muhimu. Simba inahitaji wachezaji wenye majina makubwa Afrika, na kwa nyakati zao za sasa wanaweza kusaini Zimbabwe, Zambia, Cameroon, Ghana, Mali, Ivory Coast sehemu ambazo wanaweza kupata vipaji vyenye ndoto kubwa.
Meddie amechezea klabu 12 tofauti katika miaka yake 14 la ushindani. Licha ya kuwaadhibu JKU FC, Singida United na Simba katika michuano ya SportPesa Super Cup mwanzoni mwa mwezi huu huko Nakuru, Kenya, Meddie amefunikwa mno katika ligi kuu. Amekuja Simba akiwa amefunga magoli Nane tu, lakini atavuta Mshahara usiopungua Tsh.12 Ml kwa mwezi.
Wakati mshambulizi wa Nzoia Sugar, Elvis Rupia akiongoza chati ya wafungaji bora akiwa amefunga magoli 15, Simba hawakuwa na maono ya mbali zaidi ya SportPesa Super Cup na VPL- tena kwa msaada wa Yanga wanaosaka wachezaji watakaowamudu kiuchumi.
Kama Simba walihitaji mfungaji kutoka ligi ya Kenya ambayo ni mahiri kwa kuzalisha wafungaji, ningewashauri kumsaini mmojawapo kati ya John Makwata (mfungaji bora wa ligi ya Kenya 2016 na 2017-akifunga magoli 15 kila msimu akiwa Ulinzi Stars) ama Jesse Werre (mfungaji bora wa ligi ya Kenya mwaka 2015 akiwa Tusker FC.
Pesa si ipo, tungeenda Zambia kuonana na Buildcon FC na Zesco United na kuulizia upatikanaji wa Makwata ( Buildcon), Werre ( Zesco). Kumsaini Meddie harakaharaka aada ya Yanga kugoma kumpa Mnyarwanda huyo Tsh 180 Ml- Pesa ya usajili na Tsh 12 Ml alizotaka kulipwa kama Mshahara wa kila mwezi, hii inadhihirisha Simba inaendelea kuangushwa na taratibu zao za usajili.
Inawezekana, Wawa bado ni beki bora, lakini umejiuliza kwanini aliachwa huru Azam FC na El Merreikh ya Sudan ambako alikosa nafasi ya Kucheza? Dida alihitajika Yanga ili akasahihishe makosa ya Mcameroon, Youthe Rostand katika lango lao naye Simba wakimbilia kumsaini, je, Simba walihitaji kipa mpya?
Salamba, Kaheza, Rashid wataongeza nini kipya ambacho Mohamed Ibrahim, Muzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Said Ndemla hawajakifanya? Kagere namsubiri, kumbuka hana Tuzo yoyote ya ufungaji bora katika ligi kuu, huku akiwa na magoli 11 tu katika michezo 30 ya kimataifa aliyoiwakilisha Rwanda.
Yanga wameisaidia Simba au wameiangamiza katika sajili za Dida, Wawa, Kagere, Rashid, Kaheza na Salamba?
ripoti yake Baraka Mbolembole