Mabingwa wa soka nchini Tanzania, Yanga wamesafiri kuelekea nchini Shelisheli kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya klabu ya St. Louis ya Shelisheli. Yanga imeondoka na wachezaji 20 na viongozi 10 akiwemo kocha George Lwandamina na msaidizi wake Shadrack Nsajigwa.
Katika mchezo huo, Yanga ambao ni mabingwa mara 27 wa soka nchini Tanzania wanahitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu hatua inayofuata baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza.
Katika mchezo huo, Yanga itawakosa Donald Ngoma, Yohana Mkomola, Amisi Tambwe na Abdallah Shaibu ambao wamekuwa na majeruhi ya muda mrefu. Pia taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema itawakosa wachezaji Obrey Chirwa na Thaba Kamusoko kwa sababu mbalimbali.
Ofisa Habari wa Yanga, Dismass Ten amesema nia ya timu yake ni kupata matokeo ili kufuzu hatua inayofuata.
Yanga iliondoka nchini Tanzania asubuhi ya leo na kupitia Nairobi nchini Kenya na endapo itashinda mchezo huo itachuana na El- Merreikh ya Sudan au Township Rollers ya Botswana