Klabu ya Yanga ya Tanzania leo imefuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na Welatya Dicha ya Ethiopia.
Bao la Welatya Dicha katika mchezo wa leo limefungwa na Djako Arafat katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliochezwa katika Mji wa Awasa nchini Ethiopia.
Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, kutokana na ushindi wa mabao 2-0 iliopata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa April 7.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa Yanga kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa umaarufu kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Timu nyingine zilizofuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ni Adouana Stars ya Ghana iliyoitupa nje Foisa Junior ya Madagascar.
Timu nyingine iliyofuzu hatua ya makundi ni Gor Mahia ya Kenya ambayo licha ya kufungwa mabao 2-1 na Supersports ya Afrika kusini, imefuzu kwa faida ya bao la ugenini baada ya kushinda bao 1-0 Mjini nairobi.