Pilikapilika za usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara limeanza kupamba motop baada ya Yanga kumsajili Mshambuliaji Yohana Mkomola kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo.
Mkomola alikuwemo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 cha Tanzania ambacho mwezi Juni kilicheza fainali za mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Gabon.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga Dismas Ten alisema usajili huo umefanywa kwa kutazama mustakbali wa mbele wa Yanga hususani kwa kuwekeza kwenye soka la Vijana.
“Huu ni usajili muhumu kwetu, Mkomola bado ni kijana mdogo na kikubwa ni kumjenga ili baadaye aichezee timu yetu kwa mafanikio,”alisema Ten.
Naye Mkomola amesema hiyo ni hatua muhimu kwake katika maisha ya soka kwa sababu anaamini ana nafasi kubwa ya kutamba akiwa kwenye kikosi cha Yanga.
Hata hivyo kabla ya kusajiliwa na Yanga mchezaji huyo alifanya majaribio kwenye klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Mkomola anaungana na mchezaji mwingine wa Serengeti Boys, Ramadhan Kabwili ambaye pia alisajiliwa na Yanga mwanzono mwa msimu huu.