Nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Cote D’voire na klabu ya Manchester City nchini Uingereza Yaya Toure amesema amesikitishwa sana kwa kukosa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa soka barani Afrika mwaka 2015.
Toure mwenye umri wa miaka 32, alishinda taji hilo mara nne mfulilizo mwaka 2011, 2012, 2013 na 2014.
Toure ameongeza kuwa kutokana na juhudi zake kuisadia timu yake ya taifa kunyakua ubingwa wa Afrika na klabu yake, haikuwa rahisi kuamini kukosa tuzo hiyo na kuweka historia kuwa mchezaji aliyewahi kushinda tuzo hiyo mara tano.
Mchezaji bora kutoka Gabon na anayechezea klabu ya Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang alimshinda Toure aliyepata alama 136 baada ya makocha na Wakurugenzi wa Kiufundi wa timu za taifa kupiga kura.
“Nimesikitishwa lakini haliwezi kubadilisha lolote. Nina uhakika hata Andre Ayew amesikitishwa baada ya kazi kubwa aliyofanya mwaka uliopita,” alisema Toure.
“Huu sio wakati wa kulalamika.Tutarudi na kuendelea kufanya bidii.”
Andre Ayew, kutoka Ghana na anayechezea klabu ya Swansea nchini Uingereza, alikuwa wa tatu kwa alama 112.
Aubameyang anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Gabon kuwahi kushinda taji hili baada ya kupigiwa kura na makocha pamoja na wakurugenzi wa kiufudi kutoka barani Afrika.
Mshambuliaji huyo wa Borrussia Dortmund anaongoza kwa ufungaji wa mabao katika ligi ya Bundesliga msimu huu ,na kati ya mechi 17 alizocheza amefunga mabao 18.