Mabingwa wa soka nchini Misri Zamalek FC wamebadilisha uamuzi wao wa kujiondoa katika ligi kuu ya soka nchini humo.
Zamalek mwishoni mwa juma, walitangaza hatua hiyo baada ya kufungwa na klabu ya El-Gaish mabao 3 kwa 2 mchuano ambao wanasema mwamuzi wa mchezo huo aliwaonea.
Uongozi wa klabu hiyo ulikutana siku ya Jumatatu na kubadilisha uamuzi huo kutokana na adhabu ambayo ilikuwa inawasubiri ikiwa wangeendelea na uamuzi huo.
Ikiwa Zamalek ikiendelea na mpango wake, Shirikisho la soka nchini Misri lingeipiga marufuku ya mwaka mmoja klabu hiyo na kuishusha daraja.
Aidha, mabadiliko hayo yamefanyika baada ya mashabiki wa Zamalek kusema ni vema wasijiondoe kwa sababu ni mwaka jana tu waliposhinda taji la soka nchini humo baada ya muda mrefu.
Viongozi wa Zamalek wameamua kuliandikia Shirikisho la soka nchini humo kulalamikia namna mchuano dhidi ya El-Gaish ulivyochezeshwa na refarii Mahmoud Al Banna.
Al Banna alimpa beki wa Zamalek Ali Gabr kadi nyekundu katika dakika za mwanzo za mchezo huo na kuwapa wapinzani wake penalti mbili, hatua iliyowakasirisha viongozi wa Zamalek.