Siku moja baada ya Zanzibar heroes kufanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji wanamichezo, wanasiasa na wameimwagia sifa na kuitakia kila la kheri katika mchezo wa fainali dhidi ya Kenya.
Zanzibar inayonolewa na Kocha Hemed Morocco iliitandika Uganda mabao mawili kwa moja yaliyofungwa na Mohammed Issa na Abdul Aziz Makame huku bao la kufutia machozi la Uganda likifungwa na Derrick Nsibambi.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Kikwete aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter na kusema mafanikio ya Zanzibar ni mafanikio yawatanzania wote.
Makamu wa kwanza wa rais mstaafu wa Zanzibar, Seif Sharrif hamad aliwataka vijana wa Zanzibar kukamilisha ratiba ya mashindano hayo kwa kuishinda Kenya na kutwaa ubingwa.
“Hongereni kwa kazi kubwa, sina khofu kwamba mtawafunga Kenya na kurudi na kikombe nyumbani,”aliandika Seif, ambaye pia ni katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF.
Mbunge wa Jimbo la Malindi na wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani Fifa, Ally Saleh alisema mafanikio ya Zanzibar yanatoa picha halisi kuwa wachezaji kutoka visiwa hivyo wanapaswa kupewa nafasi katika timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mchezo wa fainali baina ya Kenya na Zanzibar utachezwa kesho kwenye Uwanja wa Machakos ukitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu baina ya Burundi na Uganda.